Mama wa mtoto aliyetelekezwa anawajibika kuwasilisha shauri la matunzo ya mtoto katika vyombo vya sheria.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Seleman Rashid wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anna Mallac (Chadema) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwawajibisha wageni wanaowazalisha wanawake na kuwatelekeza ili kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na kupunguza wimbi la watoto wa mitaani.
Naibu Waziri alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, kifungu cha 43, mama wa mtoto aliyetelekezwa anawajibika kuwasilisha shauri la matunzo ya mtoto katika vyombo vya sheria.
Alifafanua “Wizara yangu kama msimamizi na mtekelezaji mkuu wa sheria hii baada ya kupokea mashauri ya aina hiyo hufanya mawasiliano na Wakala wa Kimataifa wa Huduma za Jamii ili kuweza kufanya uchunguzi na ufuatiliaji katika upande wa mlalamikiwa ambaye ndiye anayedhaniwa kuwa baba wa mtoto”.
Baada ya uchunguzi huo inapothibitishwa pasipo shaka kuwa mlalamikiwa ndiye baba halisi wa mtoto husika , taratibu za malezi , matunzo na ulinzi wa mtoto huyo hufanywa kwa kutumia ofisi za balozi za nchi husika.
Mbunge huyo wa Viti Maalumu, ambaye alisimama tena kwa swali la nyongeza alilielezea Bunge kuwa raia wa China na Uingereza wanaofanya shughuli za ukandarasi wa ujenzi wa barabara vijijini na kwenye machimbo wamewazalisha wanawake vijijini watoto na kisha kuwatelekeza na kurudi katika nchi zao.
“Wanawake hao wanahangaika na watoto wao weupe wamechakaa utawaona wameshikilia muhindi huku baba zao Wachina na Waingereza waliowazalisha wamerudi kwao je, Serikali haioni sasa itoe elimu kwa wanawake hao ili waweze kwenda kupata haki zao,” alihoji Mbunge huyo.
Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alimtaka mbunge huyo na wananchi wengine kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuzuia mimba zisizohitajika.
Katika kuelezea suala la ulinzi Naibu Waziri Afya na Ustawi wa Jamii alisema katika kuhakikisha haki za watoto walio katika mazingira hatarishi hususan watoto waliotelekezwa, wanaonyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya ukatili zinalindwa, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau wa maendeleo imeanzisha programu ya ulinzi na usalama wa mtoto ambapo mifumo ya ulinzi na usalama wa watoto imeimarishwa kwa kuundwa timu za ulinzi katika ngazi ya halmashauri, kata na vijiji na mitaa.
“Hadi sasa mifumo ya ulinzi na usalama imeanzishwa katika halmashauri za Hai, Magu, Kasulu, Temeke, Nyamagana, Ilemela, Kinondoni, Ilala, Musoma na Bukoba. Timu hizo hujumuisha wataalamu mbalimbali wanaohusika na ulinzi wa watoto wakiwemo maofisa ustawi wa jamii,” alisema.
Alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014 programu ya ulinzi na usalama itasambazwa katika halmashauri 25 hivyo kupitia programu hiyo matukio ya unyanyasaji, utelekezaji na ukatili kwa watoto utazuiwa na kushughulikiwa ipasavyo.
0 comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO HAPA....